Jumapili 15 Novemba 2026 - 12:03
Maktaba zigeuzwe kuwa vituo hai vya uzalishaji wa maarifa na ukuzaji wa fikra / Asisitiza kuthamini hadhi ya kitaaluma ya wahudumu wa maktaba

Hawza/ Ayatullah A'rafi amesisitiza umuhimu wa kugeuza maktaba za Hawza za Kielimu kuwa vituo hai vya uzalishaji, ubadilishanaji na uenezaji wa maarifa pamoja na ukuzaji wa fikra.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maelezo kamili ya ujumbe wa Ayatullah A'rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini, kwa mnasaba wa Wiki ya Kitabu na Usomaji ni kama ifuatavyo:

بسم الله الرحمن الرحیم

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Wahudumu wa maktaba, watafiti na wapitao katika njia ya elimu na maarifa,

Assalamu Alaikum

Wiki ya Kitabu na Usomaji ni fursa adhimu ya kutafakari nafasi ya msingi ya maktaba katika maisha ya kielimu ya mwanadamu na ulimwengu, pamoja na vituo vya elimu na Hawza za Kielimu, na pia kutambua upya wajibu wa taasisi za kielimu katika kuweka mazingira ya ukuaji na ustawi wa kitabu na maktaba katika hali za sasa.

Bila shaka, katika utamaduni wa kielimu wa Hawza, maktaba si mahali pa kukusanyia na kuhifadhi maandiko pekee; bali ni nguzo ya utafiti, mazingira ya mwingiliano wa fikra, na kiungo kinachounganisha urithi wa kielimu wa waliotangulia na jitihada za kielimu za kizazi cha sasa.

Ni vyema katika mnasaba huu kuyakumbuka maneno yenye nuru ya Imam Jaʿfar al-Sadiq (a.s.) aliposema:

"Andika elimu yako na uisambaze miongoni mwa ndugu zako, na vitabu vyako viwe urithi kwa watoto wako."

Mwongozo huu, pamoja na kusisitiza uenezaji wa elimu, unakumbusha pia wajibu wa kuhamisha hazina za kielimu kwa vizazi vijavyo; wajibu ambao maktaba zina nafasi ya kipekee na isiyokanushika katika kuutekeleza.

Katika muktadha huu, maktaba za Hawza zinapaswa, kwa kuzingatia hadhi ya kielimu na ujumbe wa kimaarifa wa Hawza za Kielimu, kupandishwa kutoka kuwa maghala ya kuhifadhi vyanzo vya elimu na kuwa vituo hai vya kusaidia na kuelekeza shughuli za utafiti.

Kupanua na kusasisha makusanyo ya vitabu, kuimarisha maktaba za kitaalamu, kuboresha huduma za taarifa na utafiti, kuendeleza miundombinu ya kiufundi na ya taarifa, pamoja na kuandaa rasilimali watu wenye utaalamu, ni miongoni mwa mahitaji muhimu ambayo utekelezaji wake unahitaji mipango madhubuti, uungwaji mkono endelevu na juhudi za dhati za viongozi na wasimamizi waheshimiwa wa Hawza za Kielimu.

Katika njia hii, nafasi ya wahudumu wa maktaba na wataalamu wa elimu ya taarifa na maarifa ni kubwa zaidi kuliko kupanga na kuhifadhi rasilimali za maktaba. Wao, kwa kutambua mahitaji ya kielimu ya watumiaji, kuwaongoza watafiti na kurahisisha upatikanaji wa hazina za maarifa, wanatoa mchango muhimu katika kuhuisha mchakato wa utafiti na kuinua ubora wa shughuli za kielimu.

Inafaa hadhi yao ya kitaaluma na kitaalamu ithaminiwe, na mazingira ya kunufaika zaidi na elimu pamoja na uwezo wao yaandaliwe.

Pamoja na hayo yote, maendeleo ya maktaba yatazaa matunda pale tu ambapo utamaduni wa kusoma utapata nafasi ya kudumu ndani ya maisha ya kielimu ya wanafunzi wa dini, sambamba na programu za elimu na utafiti.

Kulea wanafunzi wenye fikra pevu, wanaouliza maswali na wenye uwezo wa uchambuzi na hoja kunategemea kufunguliwa kwa upeo wa usomaji unaovuka maandiko ya darasani, kuimarishwa usomaji huru na unaolenga kutatua matatizo, na kuandaliwa kwa fursa zinazofaa za kuzoeana na kazi za kielimu na kimaarifa.

Kwa hiyo, kutambulisha vitabu vyenye thamani, kuhamasisha usomaji endelevu na kuunganisha shughuli za kielimu na usomaji wa vitabu lazima viwe miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na shule pamoja na vituo vya Hawza.

Suala jingine muhimu ni mabadiliko na mageuzi makubwa yaliyotokea katika dhana na upeo wa kitabu kutokana na maendeleo ya kushangaza ya sayansi za utambuzi na teknolojia janja, pamoja na manufaa na changamoto zake.

Suala hili na matokeo yake vinaongeza umuhimu wa kutambua upya dhana za kitabu, utafiti na uzalishaji wa kielimu, kuvijenga upya, na kuelekeza mabadiliko yajayo katika utafiti na elimu za Kiislamu.

Zaidi ya hayo, kuongoza juhudi za kufufua urithi wa maandishi ya kidini, Kiislamu na Kishia, kuhifadhi urithi wake wa kihistoria, na kuunda mtandao wa maktaba na mifumo ya taarifa ni jukumu jingine muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele.

Tunatumaini kwamba kwa ushirikiano wa wasimamizi, walimu, wahudumu wa maktaba na wenye dhamana ya masuala ya kielimu na kitamaduni, maktaba za Hawza zitapata zaidi nafasi inayostahili na kugeuzwa kuwa vituo hai vya uzalishaji, ubadilishanaji na uenezaji wa maarifa pamoja na ukuzaji wa fikra.

Vituo ambavyo kupitia hivyo taa ya elimu na maarifa itang'ara zaidi, njia ya kulea wanazuoni na watafiti wa baadaye itakuwa rahisi zaidi, na mazingira ya kuvuka hali iliyopo na kuondoa mapungufu yaliyopo kwa sasa yataandaliwa.

Ninachukua fursa hii ya kuwatakia heri ya Wiki ya Kitabu na Usomaji, na kuwashukuru kwa dhati wahudumu wa maktaba, watafiti, waandishi na wote wanaoshiriki katika kueneza utamaduni wa kusoma na kusambaza maarifa.

Pia namwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie nyote, mafanikio zaidi katika kuimarisha msingi wa kielimu wa Hawza na katika kueneza mafundisho halisi ya Uislamu.

Alireza A'rafi
Mkurugenzi wa Hawza Nchini Iran

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha